Wahamiaji waliotumia programu ya Biden waagizwa kuondoka Marekani 'mara moja'
Zaidi ya watu 900,000 waliingia Marekani kihalali na programu hii, ambayo sasa inatumika "kuwaondoa" nchini humo.
Muhtasari
- Wahamiaji waliotumia programu ya Biden waagizwa kuondoka Marekani 'mara moja'
- Viboko 50 wauawa na ugonjwa wa kimeta katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
- 'Muujiza': Mtoto wa kwanza kuzaliwa Uingereza kupitia kupandikizwa kwa kizazi
- Algeria na Mali zafungiana anga kwa safari za ndege
- Korea Kusini kufanya uchaguzi wa rais Juni 3
- Rais wa Kenya William Ruto ashutumiwa kwa kuchochea vita DRC na Sudan
- Kwanini hatukumpokea raia aliyefurushwa Marekani - Sudan Kusini
- Rais Zelensky akiri wanajeshi wake wameingia eneo linalodhibitiwa na Urusi
- China yaapa kupigana 'hadi mwisho' baada ya tishio la hivi punde la ushuru la Trump
- Watu saba wafa baada ya boti kupinduka katika Ziwa Victoria
- Watu wanne wauawa, 43 watekwa kaskazini magharibi mwa Nigeria
- Marekani inajiandaa kwa mazungumzo ya moja kwa moja ya nyuklia na Iran - Trump
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Wahamiaji waliotumia programu ya Biden waagizwa kuondoka Marekani 'mara moja'
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu ya wahamiaji walioingia Marekani wakati wa utawala wa Biden na kutumia programu maalum kupanga miadi ya kupata hifadhi wameagizwa kuondoka nchini humo "mara moja".
Takriban wahamiaji 900,000 walioingia kwenye mpaka wa kusini kwa kutumia programu, CBP One, waliruhusiwa kusalia Marekani kwa miaka miwili na kupewa fursa ingawa kwa "masharti" kutokana na sheria za uhamiaji kufanya kazi nchini humo kihalali.
Sasa, wengi wao wanafahamishwa kuwa fursa waliopewa imebatilishwa na kwamba watakabiliwa na mashtaka ikiwa watasalia Marekani.
Rais Donald Trump kwa muda mrefu ameahidi kuondoa wahamiaji wengi zaidi nchini Marekani. Utawala wake hivi majuzi ulibadilisha jina la programu kuwa CBP Home na unaitumia kwa wanaotaka "kujiondoa" wenyewe.
Soma zaidi:
Viboko 50 wauawa na ugonjwa wa kimeta katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban viboko 50 na wanyama wengine wakubwa wameuawa kwa ugonjwa wa kimeta katika mbuga kongwe zaidi barani Afrika, mkurugenzi wake amesema.
Picha zilizoshirikiwa na Mbuga ya Kitaifa ya Virunga katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zinaonyesha wanyama hao wasio tembea wakielea kando ya Mto Ishasha.
Maafisa wa Hifadhi wanasema walianza kuonekana wakiwa hivyo wiki iliyopita.
Chanzo cha ugonjwa huo hakijajulikana lakini vipimo vimethibitisha kuwepo kwa kimeta.
Mkurugenzi wa Hifadhi hiyo Emmanuel de Merode alisema kazi inaendelea ya kuchukua wanyama hao na kuwazika ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo, lakini ni vigumu kwa sababu hakuna wachimbaji.
Trump kuwapiga faini wahamiaji watakaokataa kuondoka
Chanzo cha picha, Reuters
Utawala wa Trump unapanga kuwatoza faini wahamiaji waliopewa agizo la kuondoka nchini Marekani hadi $998 kwa siku ikiwa hawataondoka nchini humo na kushikilia mali zao ikiwa hawatalipa, kulingana na hati zilizoonekana na Shirika la Reuters.
Faini hizo zinazotokana na sheria ya mwaka 1996, iliyotekelezwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2018, wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Donald Trump.
Utawala wa Trump unapanga kutumia adhabu hizo kwa muda wa hadi miaka mitano, ambayo inaweza kusababisha faini ya zaidi ya dola milioni moja, afisa mkuu wa Trump alisema, aliyeomba kutotajwa jina.
Utawala wa Trump pia unafikiria kushikilia mali ya wahamiaji ambao hawalipi faini, kulingana na barua pepe za serikali zilizoonekana na Reuters.
Katika kujibu maswali ya Reuters, msemaji wa Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani Tricia McLaughlin alisema katika taarifa yake kwamba wahamiaji nchini Marekani kinyume cha sheria wanapaswa kutumia programu ya simu iliyokuwa ikijulikana kama CBP One - iliyopewa jina la CBP Home chini ya Trump - "kujiondoa wenyewe nchini humo."
"Ikiwa hawatafanya hivyo, kuna athari watakazokabiliana nazo," McLaughlin alisema. "Hii ni pamoja na faini ya $998 kwa siku kwa kila siku ambayo mhamiaji haramu alipuuza agizo lao la mwisho la kufurushwa."
Soma zaidi:
'Muujiza': Mtoto wa kwanza kuzaliwa Uingereza kupitia kupandikizwa kwa kizazi
Chanzo cha picha, WTUK
Maelezo ya picha, Mtoto Amy Isabel aliyepigwa picha mara baada ya kuzaliwa Mtoto wa kike anayechukuliwa kuwa "muujiza" amekuwa wa kwanza nchini Uingereza kuzaliwa na mama kupitia njia ya kupandikizwa kwa kizazi.
Mama wa mtoto huyo, Grace Davidson, 36, alizaliwa bila tumbo la uzazi, na dadake akamsaidia na tumbo lake mnamo mwaka 2023 - katika kile ambacho wakati huo kilikuwa upandikizaji pekee wa uzazi uliofaulu nchini Uingereza.
Miaka miwili baada ya operesheni hiyo ya kwanza kuwahi kufanyika, Grace alijifungua mtoto wake wa kwanza mwezi wa Februari. Yeye na mumewe, Angus, 37, wamempa binti yao jina la dada yake Amy, ambaye alitoa tumbo lake la uzazi.
Kumbeba mtoto Grace - ambaye alikuwa na uzani wa zaidi ya kilo mbili kwa mara ya kwanza ilikuwa jambo la "kipekee" na "kufurahisha", mama Grace alisema.
"Haikuwa rahisi kwetu kwa sababu hatukuwahi kufikiria kwamba hili lingewezekana," anasema.
Grace na Angus, ambao wanaishi kaskazini mwa London lakini wanatoka Scotland, wanatumai kupata mtoto wa pili kwa kutumia tumbo la uzazi lililopandikizwa.
Awali wanandoa hao walitaka kusalia bila kujulikana, lakini kufuatia kuzaliwa salama kwa mtoto Amy sasa wamezungumza na BBC kuhusu "muujiza" huo uliotokea.
Timu ya upasuaji iliiambia BBC kuwa wamefanya upandikizaji wa uzazi mwingine mara tatu kwa kutumia tumbo la uzazi l a waliofariki ambao walikuwa wameridhia tangu kupandikizwa kwa Grace.
Wanalenga kutekeleza jumla ya upandikizaji 15 kama sehemu ya majaribio ya kimatibabu.
Soma zaidi:
Algeria na Mali zafungiana anga kwa safari za ndege
Chanzo cha picha, AFP
Algeria na Mali kila moja zimefunga anga lao kwa safari za ndege kutoka nchi nyingine, huku mzozo kuhusu ndege isiyo na rubani iliyotunguliwa karibu na mpaka wao wa pamoja ukiongezeka.
Siku ya Jumapili, bila kutoa ushahidi, Mali ilishutumu jirani yake wa kaskazini kwa kuwa mfadhili na msafirishaji wa ugaidi baada ya Algeria kushambulia moja ya ndege zake zisizo na rubani wiki iliyopita.
Algeria ilikuwa ya kwanza kupiga marufuku safari za ndege kwenda na kutoka Mali, kisha Mali baadaye ilisema ilikuwa ikifanya vivyo hivyo kwa safari zote za ndege za Algeria "kwa usawa".
Taarifa ya Jumapili yenye maneno makali kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya Mali ilipinga maelezo ya awali ya Algeria kwamba ndege hiyo ya uchunguzi isiyokuwa na rubani ilikiuka anga yake.
Taarifa hiyo ilielezea kuangushwa kwa ndege hiyo isiyo na rubani kama "hatua ya kiuadui iliyopangwa". Algeria ilielezea madai hayo kuhusu ugaidi kuwa "yasiyo na uzito [na kwamba]... hayana budi kutozingatiwa au kujibiwa".
Wanajeshi wa Mali wanapambana na watu wanaotaka kujitenga kwa kabila la Tuareg kaskazini mwa Mali. Wana ngome katika mji wa Tinzaoutin, unaozunguka mpaka wa Mali na Algeria.
Kutunguliwa kwa ndege hiyo isiyo na rubani kumeibua mvutano wa kidiplomasia, huku Mali, pamoja na washirika wake Niger na Burkina Faso, wakiwaita mabalozi wao kutoka Algiers.
Mwaka jana, nchi hizo tatu zinazoongozwa na jeshi ziliunda kambi ya kikanda, Muungano wa Mataifa ya Sahel.
Mali mara kwa mara inaishutumu Algeria kwa kutoa hifadhi kwa makundi yenye silaha ya Tuareg.
Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika iliwahi kuwa mpatanishi mkuu wakati wa zaidi ya muongo mmoja wa vita kati ya Mali na wanaotaka kujitenga.
Uhusiano wao umedorora tangu 2020 baada ya jeshi kuchukua mamlaka huko Bamako.
Hivi karibuni Algeria iliweka wanajeshi kwenye mipaka yake ili kuzuia kupenya kwa wanamgambo na silaha kutoka kwa vikundi vya kijihadi vinavyoendesha harakati zao nchini Mali na nchi zingine za eneo la Sahel la Afrika Magharibi.
Pia unaweza kusoma:
Korea Kusini kufanya uchaguzi wa rais Juni 3
Chanzo cha picha, Getty Images
Korea Kusini itafanya uchaguzi wa rais tarehe 3 Juni, kaimu kiongozi wake amesema, baada ya mahakama ya kikatiba ya nchi hiyo kuunga mkono hoja ya kumwondoa aliyekuwa Rais Yoon Suk Yeol.
Bunge la nchi hiyo lilipitisha hoja ya kumuondoa madarakani Rais Yoon mnamo mwezi Desemba kwa kutangaza sheria ya kijeshi iliyoshtua nchi.
Mahakama iliidhinisha kushtakiwa kwake tarehe 4 Aprili, na hivyo kufungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi wa haraka ndani ya siku 60.
Kaimu rais Han Duck-soo alitangaza tarehe ya uchaguzi Jumanne, akisema nchi inahitaji "kupona haraka" na kusonga "mbele".
Tangazo la Yoon la sheria ya kijeshi liliitumbukiza Korea Kusini katika hali ya sintofahamu ya kisiasa na kusababisha mgawanyiko mkubwa nchini humo.
"Ninaomba radhi kwa kuleta mkanganyiko na wasiwasi kwa wananchi katika kipindi cha miezi minne iliyopita, na kwa kukabiliwa na hali hii ya kusikitisha katika nafasi ya urais," Han alisema.
Yoon alirejelea vitisho kutoka kwa "vikosi vinavyopinga serikali" na Korea Kaskazini alipotangaza sheria ya kijeshi. Lakini baada ya muda mfupi kupita, ilibainika wazi kuwa hatua hiyo haikuchochewa na vitisho vya nje bali matatizo yake ya kisiasa ya ndani.
Ameshtakiwa kwa kosa tofauti la uasi mbele ya mahakama ya jinai.
Soma zaidi:
Rais wa Kenya William Ruto ashutumiwa kwa kuchochea vita DRC na Sudan
Chanzo cha picha, EPA
Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amezitaka jamii za kimataifa kumuwekea vikwazo Rais wa Kenya William Ruto kwa tuhuma za kuchochea mizozo nchini Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kulinda maslahi yake ya kibiashara.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha KTN usiku wa kuamkia leo, Gachagua alidai kuwa Rais Ruto anashirikiana na wanamgambo wa RSF wa Sudan, Mohammed Hamdan Dagalo (Hemedti), pamoja na viongozi wa kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda, kwa lengo la kulinda mtandao wa biashara ya dhahabu.
“Nataka kuomba jamii ya kimataifa wazingatie hali hii nchini kwetu. Hatutapata amani wala usalama katika eneo hili endapo hatutamdhibiti Rais William Ruto, ambaye amejaa ubinafsi na tamaa ya kujinufaisha kibiashara katika kanda hii,” alisema Gachagua.
Aliongeza, “Kwa vifo vinavyotokea Sudan, kamanda halisi wa RSF si Hemedti, bali ni William Ruto, kwa sababu ili harakati yoyote ifanikiwe, inahitaji rasilimali. Pesa za dhahabu zinazotokana na Kenya zinatumika kununua silaha na kuua wanawake na watoto.”
Kauli hii ilitolewa siku moja baada ya serikali ya Sudan inayoongozwa na jeshi kupinga mkutano ulipangwa kufanyika London, ikikosoa kutoshirikishwa kwake na mwaliko wa Kenya, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Chad, nchi ambazo Sudan inazishutumu kwa kushiriki katika mzozo huo.
Mnamo mwezi Februari, Sudan iliishutumu Kenya kwa kuwawezesha makundi yanayohusiana na RSF kusaini mkataba wa kisiasa kwa ajili ya kuanzisha serikali mbadala.
Pia unaweza kusoma:
Kwanini hatukumpokea raia aliyefurushwa Marekani - Sudan Kusini
Chanzo cha picha, Getty Images
Sudan Kusini imesikitia uamuzi wa Marekani wa kubatilisha viza zinazomilikiwa na raia wake wanaotaka kuingia Marekani kutokana na mzozo wa uhamiaji licha ya wao kuwa tayari kushirikiana na Washington.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Kigeni kupitia mtandao wa Facebook mwanamume ambaye walimkataa kumpokea kuingia nchini humo tarehe 6 mwezi huu baada ya kufukuzwa kwa kukosa kibali cha kuishi Marekani alikuwa ni raia wa DRC na sio raia wake kama ilivyosemekana.
‘’Rekodi ambazo wanazo zinaonyesha kuwa Bwana Makula Kintu aliyezaliwa mwaka 1977 mwezi Aprili tarehe 2 ni raia wa Kongo na sio Sudan Kusini,’’ Wizara hiyo ilisema.
"Serikali ya Sudan Kusini inaelezea masikitiko yake kwa hali iliyosababisha hali hii."
Tarehe 5 Aprili, Marekani ilibatilisha viza zote zilizokuwa na wamiliki wa pasipoti wa Sudan Kusini kutokana na "kushindwa" kwa taifa hilo la Afrika "kukubali kurejeshwa kwa raia wake kwa haraka".
Utawala wa Rais wa Amerika Donald Trump umechukua hatua kali za kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kuwarejesha makwao watu wanaoaminika kuwa Marekani kinyume cha sheria.
Utawala huo umeonya kwamba nchi zitakazoshindwa kuwapokea raia wao kwa haraka zitachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kuwekewa vikwazo vya visa au ushuru wa forodha.
Pia unaweza kusoma:
Rais Zelensky akiri wanajeshi wake wameingia eneo linalodhibitiwa na Urusi
Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amekiri hadharani kwa mara ya kwanza kwamba vikosi vya Ukraine viko katika eneo la Belgorod, Urusi.
Katika hotuba yake aliyoitoa Jumatatu, Zelensky alisema, “Tunaendelea kufanya operesheni za kijeshi katika maeneo ya mipakani kwenye ardhi ya adui, na hiyo ni haki kabisa - vita lazima virejee mahali vilipotokea.”
Kauli hii pia ilihusiana na eneo la Kursk, ambapo Ukraine inashikilia sehemu ndogo baada ya shambulizi kubwa mwaka jana, ingawa Moscow imechukua tena udhibiti wa sehemu kubwa ya eneo hilo.
Zelensky alifafanua kuwa lengo kuu la operesheni hizo ni kulinda maeneo ya mipaka ya Sumy na Kharkiv, na kupunguza shinikizo katika maeneo mengine ya mstari wa mbele, hasa katika eneo la mashariki la Donetsk.
Jeshi la Urusi liliripoti mwezi uliopita kwamba Ukraine ilijaribu kuvuka mpaka na kuingia kwenye eneo la Belgorod, lakini walidai kuwa mashambulizi hayo yalizuiwa kwa mafanikio.
Rais Zelensky alithibitisha kuwa operesheni za kijeshi za Ukraine katika maeneo ya Kursk na Belgorod ni sehemu ya juhudi za kulinda nchi yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Mnamo tarehe 18 Machi, Zelensky alikiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba vikosi vya Ukraine viko kwenye eneo la Belgorod, akisema “Kuna operesheni inayoendelea huko,” alipoulizwa kuhusu taarifa za Urusi zinazosema kuwa vikosi vya Ukraine vilijaribu kuingia sehemu ya magharibi ya Belgorod bila mafanikio.
Taarifa za hivi karibuni kutoka kwa wanablogu wa kijeshi wa Urusi zinaonyesha kuwa vikosi vya Ukraine vinajiondoa kutoka eneo la Demidovka, likionyesha kuwa operesheni za Ukraine katika eneo hili ni za kiwango kidogo ikilinganishwa na zile za Kursk, ambapo Ukraine ilishinda vijiji vingi, ikiwemo mji wa Sudzha.
Hali hii pia inaweza kumaanisha kuwa Ukraine inatumai kubadilishana maeneo ya Urusi inayoshikilia kwa sehemu za maeneo ya Ukraine yanayoshikiliwa na Moscow katika mazungumzo yoyote ya amani ya baadaye.
Wachambuzi wa vita, hasa kutoka Ukraine na Magharibi, wamehoji ufanisi wa kijeshi wa operesheni hizi za Ukraine kwenye ardhi ya Urusi, wakibaini idadi kubwa ya majeruhi na changamoto za upatikanaji wa silaha.
Pia unaweza kusoma:
China yaapa kupigana 'hadi mwisho' baada ya tishio la hivi punde la ushuru la Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
China imesema itapambana vilivyo na nyongeza mpya ya ushuru kutoka kwa Marekani huku mataifa hayo mawili yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani yakiwa karibu kuingia katika vita vikali vya kibiashara.
China imeishutumu Marekani kwa manyanyaso baada ya Rais Donald Trump kusema atatangaza nyongeza nyingine ya asilimia hamsini juu kwa bidhaa kutoka China iwapo nchi hiyo haitabatilisha uamuzi wake wa kuziongezea ushuru bidhaa za Marekani.
Kwa upande wake wizara ya biashara ya Beijing imesema kuwa haitakubali kamwe ‘’kushinikizwa na Marekani’’ na kuapa itapigana hadi mwisho.
Ushuru huo mpya unaweza kuacha baadhi ya makampuni ya Marekani yanayoleta bidhaa fulani kutoka China yakikabiliwa na ushuru wa asilimia 104%.
Licha ya Vietnam kuathirika zaidi na ushuru wa Trump, Waziri Mkuu wa Vietnam Pham Minh Chinh anasema nchi hiyo itanunua bidhaa zaidi kutoka Marekani, zikiwemo bidhaa zinazotumika kwa usalama na ulinzi.
kwa uagizaji wa magari kutoka Japani na kile kinachojulikana ushuru wa asilimia 24% kwa bidhaa zingine za Japani.
Rais Trump pia amesema hana nia ya kusitisha nyongeza alizotangaza kwa karibu kila nchi duniani licha ya masoko ya hisa kuporomoka.
Pia unaweza kusoma:
Watu saba wafa maji baada ya boti kupinduka katika Ziwa Victoria
Takriban watu saba wanahofiwa kufariki baada ya boti ya mizigo waliyokuwa wakisafiria kutoka kisiwa cha Kalangala nchini Uganda kupigwa na upepo mkali na kupinduka kwenye Ziwa Victoria.
Watu watano waliokolewa na mashua ya wavuvi.
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani mkasa huo ulitokea alfajiri ya Jumatatu, saa 3:00 asubuhi.
Boti hiyo ilikuwa imebeba mkaa kutoka kisiwa cha Kalangala hadi jiji la Entebbe lililo kando ya ziwa kubwa zaidi la maji safi barani Afrika.
Mmoja wa walionusurika, Moses Bukenya, alisema walikuwa watu kumi na wawili ndani ya boti hiyo iliyoharibika.
"Kabla ya mashua kupinduka, coxswain alituambia kwamba maji yalikuwa yakijaa kwenye boti, na tukaanza kurusha mifuko ya mkaa baharini. Hata hivyo, mashua hatimaye ilipinduka, manusura walio hai waking'ang'ania magunia ya mkaa," alisimulia katika mahojiano na Gazeti la eneo hilo, New Vision.
Katika miaka ya hivi karibuni, usafiri wa majini nchini Uganda umekumbwa na majanga.
Mnamo 2023, takriban watu ishirini walikufa baada ya boti ya abiria iliyojaa kupita kiasi kupinduka katika Ziwa Victoria. Vile vile mwaka 2018 mwezi Novemba boti lilipinduka na kuua abiria 30 katika Ziwa Viktoria.
Pia unaweza kusoma:
Watu wanne wauawa, 43 watekwa kaskazini magharibi mwa Nigeria
Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi katika Jimbo la Katsina kaskazini magharibi mwa Nigeria, wamesema watu 43 wametekwa nyara katika kijiji kimoja, huku wengine wanne wakiuawa katika shambulio baya.
Inakuja chini ya wiki moja baada ya Jenerali wa Jeshi la Nigeria kuachiliwa baada kuzuiliwa karibu miezi miwili na watekaji nyara.
Katsina, jimbo analotoka Rais wa zamani wa Nigeria Muhammadu Buhari, limeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya majambazi na watekaji nyara ambayo yamegharimu maisha ya watu wengi.
Katika shambulio hilo la Jumapili usiku, wakaazi walisema kuwa watu wanaoshukiwa kuwa majambazi waliokuwa wakiendesha pikipiki waliwavamia wakaazi wakiwapiga risasi kabla ya kuwateka nyara waathiriwa.
Baadhi ya wanakijiji walipigwa risasi na kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Polisi wanasema msako unaendelea ili kuwaokoa waathiriwa na kuwakamata wahusika.
Pia unaweza kusoma:
Marekani inajiandaa kwa mazungumzo ya moja kwa moja ya nyuklia na Iran - Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani na Iran zitafanya mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu makubaliano ya nyuklia siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa Rais Donald Trump.
Mkutano huo pia umethibitishwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, ambaye amesema kuwa ni fursa kubwa ambayo pia inakabiliwa mtihani mkubwa.
Rais Trump alisema kuwa mazungumzo hayo yatafanyika katika ngazi cha juu sana na kuonya kuwa, ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa, itakuwa “siku mbaya sana kwa Iran.”
Mwezi uliopita, Trump alionyesha uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran baada ya kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kukataa hadharani pendekezo la mazungumzo ya moja kwa moja.
Rais Trump alifichua habari za mazungumzo hayo baada ya mkutano na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye amekuwa akisisitiza haja ya kuzuia Iran isifanye maendeleo katika silaha za nyuklia.
“Iran haiwezi kuwa na silaha za kinyuklia, na kama mazungumzo haya hayatakuwa na mafanikio, nadhani itakuwa siku mbaya kwa Iran.”Trump alisema haya akiwa ofisini kwake.
Hata hivyo, Rais Trump aliepuka kutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo hayo, kama vile ni viongozi gani watahusika au ni hatua zipi zilizofikiwa hadi sasa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alithibitisha kuwa mkutano huo utafanyika huko Oman tarehe 12 Aprili.
Kupunguza uwezo wa Iran katika uzalishaji wa silaha za kinyuklia kumekuwa ni lengo kuu la sera za kigeni za Marekani na washirika wake kwa miongo kadhaa.
Katika mwaka 2015, Rais Barack Obama alifanikisha makubaliano na Iran, ambayo ilikubali kupunguza shughuli zake za kinyuklia na kuruhusu wakaguzi wa kimataifa ili kuhakikisha vifaa vinatumika kwa madhumuni ya kiraia pekee, na sio kwa ajili ya uzalishaji wa silaha.
Hata hivyo, mwaka 2016, Trump alijiondoa kutoka kwa makubaliano hayo, akielezea kushinikiza kurekebisha makubaliano hayo.
Katika miaka iliyofuata, Iran ilikiuka masharti ya makubaliano hayo, na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeonya kuwa Iran imejilimbikizia hifadhi kubwa za urani ya kutajirika, ambayo inaweza kutumika kutengeneza mabomu ya kinyuklia.
Israel, kwa upande wake, inaona kuwa kuzuia Iran kupata silaha za kinyuklia ni jambo muhimu sana kwa usalama wake wa muda mrefu.
Inaripotiwa kwamba imekuwa ikifikiria kushambulia vituo vya uzalishaji vya Iran katika miezi ya hivi karibuni. Mwaka jana, Israel ilisema kuwa ilishambulia tovuti ya kinyuklia ya Iran kwa kulipiza kisasi kwa shambulizi la makombora kutoka Iran dhidi ya Israel.
Netanyahu, akizungumza katika Ikulu ya White House, alisema: “Sisi na Marekani tumeungana katika lengo kwamba Iran isipate silaha za kinyuklia kamwe.
Ikiwa hili linaweza kufanywa kidiplomasia, kama ilivyofanyika Libya, nadhani hiyo itakuwa hatua nzuri.” Makubaliano haya yanaashiria safari ndefu na ngumu katika juhudi za kimataifa za kudhibiti silaha za kinyuklia za Iran.
Kila upande unalenga kuonyesha msimamo wake, huku mamilioni ya watu wakiwa wameshika pumzi, wakisubiri kuona kama tahadhari za kisiasa na kidiplomasia zitafanikiwa au kama mlango wa vita utalipuka.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo, na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja