Ukraine yang'ang'ana kuweka 'ukuta wa droni' kukabiliana na mashambulizi ya Urusi
Urusi imeongeza kasi ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kote Ukraine mwezi huu katika juhudi za kupunguza ari ya Waukraine katika vita.
Muhtasari
- Ukraine yang'ang'ana kuweka 'ukuta wa ndege zisizo na rubani' kukabiliana na mashambulizi ya Urusi
- Wachezaji maarufu walioaga vilabu vyao mwaka huu
- Lamine Yamal aongeza mkataba na Barcelona hadi 2031
- Mahakama ya Marekani yasitisha ushuru wa Trump
- Muhamiaji akamatwa kwa kuandika barua ya kutishia kumuua Trump
- Mama mzazi aliyemuuza binti yake kwa mganga afungwa maisha
- Israel yatangaza ujenzi mkubwa wa makazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina
- Andrew na Tristan Tate wafunguliwa mashitaka 21 nchini Uingereza
- Daktari mstaafu jela kwa kubaka mamia ya wagonjwa wakiwemo watoto
- Klabu ya Man Utd yazomewa baada ya kushindwa huko Malaysia
- Wanafunzi 'wanajuta' kutuma maombi katika vyuo vya Marekani
- Elon Musk aondoka Ikulu ya White House, atangaza DOGE kuendelea
- Mahakama ya Biashara Marekani yasema Trump alikiuka mamlaka yake kutoza ushuru karibu kila nchi
- Ghala la chakula Gaza lavamiwa na 'makundi ya watu wenye njaa' - WFP
- Trump aonekana kumuwekea Putin makataa ya 'wiki mbili' juu ya suala la Ukraine
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Rashid Abdallah
Ukraine yang'ang'ana kuweka 'ukuta wa droni' kukabiliana na mashambulizi ya Urusi
Maelezo ya picha, Ndege ya droni aina ya Raybird ina uwezo wa kuruka bila kusimama zaidi ya kilomita 1,000 ili kufanya oupelelezi na kugonga shabaha ndani ya Urusi. Urusi imeongeza kasi ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kote Ukraine mwezi huu katika juhudi za kupunguza ari ya Waukraine katika vita - lakini pia inazidisha mashambulizi ya ardhini katika maeneo mengi ya mstari wa mbele, kulingana na maafisa na wachambuzi wa Ukraine.
Baadhi ya mashambulizi hayo yamefaulu, huku wanajeshi wa Ukraine walioko Donetsk na kaskazini wakilazimika kurudi nyuma kutoka kwa baadhi ya maeneo, huku baadhi ya maeneo ya vijijini kusini pia yamechukuliwa na Urusi.
Lakini utumiaji ulioimarishwa wa Ukraine wa ndege zisizo na rubani, zilizowekwa katika maeneo kadhaa kwenye uwanja wa vita, umeisaidia Kyiv kusababisha hasara kubwa kwa vikosi pinzani na hasara ndogo kwa wanajeshi wake. Mashambulizi hayo yanaweza kuwa mabaya zaidi katika miezi ijayo.
Wananchi wa Ukraine wanajaribu kupanua tasnia yao ya ndege zisizo na rubani ili kuunda eneo la kujihami kwenye sehemu muhimu za mstari wa mbele, ambayo mara nyingi huitwa "ukuta wa droni."
Wakati huo huo, ikipuuza juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump za kupata usitishaji mapigano, Kremlin inafuata mkakati wa pande mbili unaolenga kuilazimisha Ukraine kukubali kushindwa - kuharibu miji yake kutoka angani na kuvunja ngome zake za ulinzi ardhini.
Anusurika kifo baada ya parachuti kumpaisha kimakosa mita 8000 kwenda juu
Chanzo cha picha, sixthtone
Mwanaume mmoja raia wa China, amenusurika kifo baada ya miamvuli ya parachuti kupaa na kumrusha kimakosa umbali wa mita 8,500 (futi 27,800) angani kaskazini-magharibi mwa China, inasema ripoti ya vyombo vya habari vya serikali.
Peng Yujiang, 55, alikuwa akifanya majaribio ya vifaa vipya akiwa juu ya milima ya Qilian umbali wa mita 3,000 usawa wa bahari, pale alipojikuta miamvuli hiyo inavutwa mita nyingine 5,000 kwenda juu hadi kwenye mawingu.
Tukio hilo la Jumamosi lilirekodiwa kwenye kamera ambayo iliwekwa kwenye parachuti la Peng na video hiyo imesambaa baada ya kuchapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Douyin, toleo la China la TikTok.
Inamuonyesha Peng akiwa kamba za mwamvuli, huku uso wake na sehemu kubwa ya mwili wake vikiwa vimefunikwa na barafu.
"Kila kitu kilikuwa cheupe. Sikuweza kuona mwelekeo wowote. Bila dira, nisingejua ni njia gani nakwenda. Nilidhani nilikuwa nikipaa kawaida, lakini kumbe, nilikuwa nikizunguka," aliambia China Media Group.
Peng alinusurika kifo kwani kuna uhaba wa oksijeni kwenye umbali huo, unaokaribia kilele cha Mlima Everest ambacho kipo ni mita 8,849. Nyuzi joto hushuka hadi -40C.
"Nilitaka kushuka, lakini sikuweza. Liliniinua juu zaidi hadi nilipokuwa ndani ya wingu," alisema.
Peng, ambaye amekuwa akisafiri kwa parachuti kwa muda wa miaka minne na nusu, alisema huenda alipoteza fahamu wakati wa kushuka kwake, na kuongeza kuwa wakati wa kutisha zaidi ni pale alipojaribu kurejesha udhibiti wa parachuti lilipokuwa likizunguka angani.
Serikali ya China inachunguza tukio hilo na Peng amesimamishwa kupaa kwa muda wa miezi sita kwa sababu safari hiyo halikuwa imeidhinishwa, limesem shirika la serikali la Global Times.
Peng hakuwa na nia ya kuruka siku hiyo na alikuwa akifanya tu majaribio ya parachuti yake ardhini, limesema Global Times.
Lakini upepo mkali ulimwinua kutoka ardhini na ukamvuta kwa nguvu, hadi akajikuta mawinguni.
Wachezaji maarufu walioaga vilabu vyao mwaka huu
Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati msimu wa soka barani Ulaya ukielekea ukingoni, baadhi ya wachezaji mashuhuri wameaga vilabu vyao.
Wachezaji hawa wamekuwa wachezaji muhimu katika timu zao kwa miaka mingi na inaaminika kuwa historia haitasahau athari zao katika maendeleo ya timu zao.
Hawa ni baadhi yao:
Kevin De Bruyne
Chanzo cha picha, PA Media
Maelezo ya picha, Kevin De Bruyne ni mwanasoka wa Ubelgiji ambaye anacheza kama kiungo wa kati na ni nahodha wa Manchester City na nchi yake ya Ubelgiji. Inasemekana anaweza kwenda Napoli, Marekani au uarabun Luka Modric
Chanzo cha picha, Real Madrid/Facebook
Maelezo ya picha, Kiungo huyo wa kati wa Croatia tayari amewaaga mashabiki wa Real Madrid kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu katika mechi ya mwisho ya La Liga ya timu hiyo, ambayo timu hiyo iliichapa Real Sociedad 2-0 Jumamosi, Mei 24, 2025. Luka Modric mwenye umri wa miaka 39, ameichezea Real Madrid mechi 590 tangu 2012. Kwa sasa yuko kwenye kikosi cha Real Madrid kitakachocheza Kombe la Dunia la Klabu ya Fifa. Alexander-Arnold
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Trent John Alexander-Arnold ni mchezaji wa kulipwa wa Uingereza ambaye anacheza kama beki wa kushoto, au wakati mwingine kama mlinzi wa kati. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alitumia miaka 20 katika klabu ya Liverpool, ambapo aliichezea klabu hiyo mechi 354 hadi mwisho wa msimu. Mkataba wake na Liverpool unamalizika mwishoni mwa msimu huu na amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na miamba ya Uhispania Real Madrid. Lucas Vázquez
Chanzo cha picha, Real Madrid/Facebook
Maelezo ya picha, Lucas Vázquez alijiunga na timu ya vijana ya Real Madrid mwaka 2007, akiwa na umri wa miaka 16, na baadaye akatolewa kwa mkopo Espanyol. Alirejea Real mwaka 2015, safari hii akijiunga na timu ya wakubwa, ambako aliendelea kucheza hadi mwisho wa msimu mkataba wake na Real ulipomalizika. Lamine Yamal aongeza mkataba na Barcelona hadi 2031
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Lamine Yamal Lamine Yamal amesaini mkataba utakaomuwezesha kuendelea kubakia na FC Barcelona hadi mwaka 2030, klabu hiyo ilitangaza Jumanne ,
Maelezo ya mkataba huo - ambao ulitiwa saini katika ofisi za klabu mbele ya rais Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo Deco - hayakutolewa na Barca, lakini ripoti nyingi kutoka kwa vyombo vya habari vya Uhispania zinasema kwamba kijana huyo nyota wa soka mwenye umri wa miaka 17, anatarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa pesa nyingi zaidi kwenye kikosi na uwezekano wa mshahara wa kila mwaka wa takriban euro milioni 19 (kama dola milioni 21) baada ya kukatwa ushuru.
Unaweza pia kusoma:
Mahakama ya Marekani yasitisha ushuru wa Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama ya shirikisho nchini Marekani imesitisha ushuru mkubwa uliowekwa na Rais Donald Trump hatua ambayo ni pigo kubwa kwa sehemu muhimu ya sera zake za kiuchumi.
Mahakama ya Kimataifa ya Biashara iliamua kwamba sheria ya dharura, ambayo Ikulu ya White House iliitisha, haimpi rais mamlaka ya upande mmoja ya kutoza ushuru kwa takriban nchi zote duniani.
Mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini Manhattan ilithibitisha kuwa Katiba ya Marekani inalipa baraza la Congress mamlaka ya kipekee ya kudhibiti biashara na nchi nyingine, na kwamba jukumu la rais la kulinda uchumi halichukui nafasi ya mamlaka hayo.
Mahakama pia ilisitisha ushuru tofauti ambao Trump aliziwekea China, Mexico, na Canada tangu arejee Ikulu ya White House, kujibu kile alichokitaja kuwa utitiri usiokubalika wa dawa za kulevya na wahamiaji haramu nchini Marekani.
Muhamiaji akamatwa kwa kuandika barua ya kutishia kumuua Trump
Chanzo cha picha, DHS
Maelezo ya picha, Ramon Morales-Reyes, 54, ni raia wa Mexico Mhamiaji wa Marekani ambaye hakuwa na vibali amekamatwa baada ya kutuma barua iliyoandikwa kwa mkono kwa serikali akisema amepanga kumuua Rais Donald Trump, wamesema maafisa.
Mwanaume huyo, Ramon Morales-Reyes, mwenye umri wa miaka 54, alisema katika barua hiyo "atampiga risasi rais kwenye kichwa" kabla ya kurudi katika nchi yake ya asili ya Mexico.
Sasa yuko katika kizuizi cha Maafisa wa Uhamiaji (ICE) huko Wisconsin.
Reyes alikuwa na rekodi ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kukamatwa mara kadhaa na kujaribu kuingia Marekani kinyume cha sheria, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani (DHS).
Maafisa wa usalama walisema mamlaka ilipokea barua hiyo kutoka kwa Reyes tarehe 21 Mei. Barua hiyo iliyoandikwa kwa wino wa buluu kwenye karatasi, inasema: "Tumechoshwa na rais huyu kutuchafua sisi Wamexico."
"Amekuwa akiifukuza familia yangu na nadhani ni wakati wa Donald J. Trump kupata adhabu."
Mstari wa mwisho wa barua hiyo unasema: "Nitaonana naye kwenye moja ya mikutano yake mikubwa."
Reyes alikamatwa siku moja baada ya barua hiyo kupokelewa.
Kulingana na maafisa, alijaribu kuingia Marekani kinyume cha sheria mara tisa kati ya 1998 na 2005, na aliwahi kukamatwa kwa kosa la uhalifu na kukimbia.
Pia unaweza kusoma:
Mama mzazi aliyemuuza binti yake kwa mganga afungwa maisha
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kelly Smith alikataa kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya wiki sita Mwanamke wa Afrika Kusini aliyepatikana na hatia ya kumteka nyara na kumsafirisha bintiye mwenye umri wa miaka sita amehukumiwa kifungo cha maisha jela pamoja na washirika wake wawili.
Racquel "Kelly" Smith, mpenzi wake Jacquen Appollis na rafiki yao Steveno van Rhyn vinakuja zaidi ya mwaka mmoja baada ya Joshlin Smith kutoweka nje ya nyumba yake huko Saldanha Bay, karibu na Cape Town.
Licha ya utaftaji uliotangazwa sana wa msichana huyo, ambaye alitoweka Februari 2024, bado hajapatikana.
Hukumu hiyo inafuatia kesi ya wiki sita huko Afrika Kusini, huku mashahidi na waendesha mashtaka wakitoa madai kadhaa ya kushtua.
Jaji Nathan Erasmus amesema, “kwa shtaka la kusafirisha binadamu unahukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa shtaka la utekaji nyara unahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela," alisema huku akishangiliwa kwa sauti kubwa mahakamani hapo.
Smith, 35, na washirika wake hawakuonyesha hisia zozote wakati hukumu zao zikisomwa katika kituo cha jamii huko Saldanha ambapo kesi ilifanyika ili kuwaruhusu wakaazi wa eneo hilo kuhudhuria kesi.
Hisia zilikuwa juu kabla ya hukumu hiyo, huku wanajamii wenye hasira wakisema watatu hao wanapaswa kupata "hukumu kali kwa sababu wanastahili".
Kabla ya hukumu, Nyanya yake Joshlin, Amanda Smith-Daniels, kwa mara nyingine tena alimsihi binti yake "mrudishe mjukuu wangu au niambie yuko wapi."
Wakati wa kesi hiyo, mahakama ilisikiliza ushahidi kutoka kwa mashahidi zaidi ya 30, ambao walieleza picha ya maisha ya shida ya msichana huyo na kutoweka baadaye.
Kelly Smith na washirika wake walikataa kutoa ushahidi au kuita mashahidi wowote kwa ajili ya utetezi wao.
Ushahidi pia ulitoka kwa Lourentia Lombaard, rafiki na jirani wa Smith ambaye aligeuka kuwa shahidi wa serikali.
Bi Lombaard alidai kuwa Smith alimwambia kuwa amefanya "kitu cha kijinga" na kumuuza Joshlin kwa mganga wa kienyeji, anayejulikana nchini Afrika Kusini kama "sangoma".
"Mtu ambaye [aliyedaiwa kumchukua] Joshlin alimtaka kwa macho na ngozi yake," Bi Lombaard aliambia mahakama.
Mchungaji wa eneo hilo alitoa ushuhuda kwamba mwaka 2023, alimsikia Smith - mama wa watoto watatu - akizungumzia kuwauza watoto wake kwa randi 20,000 ($1,100; £850) kila mmoja, ingawa alisema yuko tayari kukubali kiwango cha chini cha $275.
Mwalimu wa Joshlin alidai mahakamani kwamba Smith alimwambia wakati wa upekuzi kwamba binti yake alikuwa tayari "kwenye meli, ndani ya kontena, na alikuwa njiani kuelekea Afrika Magharibi."
Pia unaweza kusema:
Israel yatangaza ujenzi mkubwa wa makazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Mawaziri wa Israeli wanasema kituo hiki cha walowezi huko Homesh kitahalalishwa Mawaziri wa Israel wanasema makaazi mapya 22 ya Walowezi wa Kiyahudi yameidhinishwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu – huu utakuwa ni upanuzi mkubwa zaidi katika miongo kadhaa.
Baadhi ya makazi hayo tayari yameshajengwa na Walowezi bila idhini ya serikali, lakini sasa yatafanywa kuwa halali chini ya sheria za Israeli, kulingana na Waziri wa Ulinzi Israel Katz na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich.
Suala la makazi ya Walowezi - ambayo ni haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israeli inapinga hili – na ni moja ya mambo yenye mzozo kati ya Israel na Wapalestina.
Katz alisema hatua hiyo "inazuia kuanzishwa kwa taifa la Palestina ambalo litahatarisha usalama wa Israel," huku ofisi ya rais wa Palestina ikisema "huko ni kuongeza mvutano hatari."
Shirika la kufatilia makazi ya Walowezi la Israel Peace Now lilisema makazi mapya "yatabadilisha kwa kiasi kikubwa Ukingo wa Magharibi na kuongeza uvamizi zaidi."
Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi 700,000 tangu ilipokalia Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki baada ya vita vya Mashariki ya Kati vya 1967 - ardhi ambayo Wapalestina wanataka kuwa sehemu ya taifa lao la baadaye.
Pia unaweza kusoma:
Andrew na Tristan Tate wafunguliwa mashitaka 21 nchini Uingereza
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Maafisa wa Romania wakiwa na Andrew Tate nje ya makazi yake huko Pipera, Ilfov, Romania, tarehe 21 Agosti 2024. Andrew Tate anakabiliwa na mashtaka 10 ya uhalifu nchini Uingereza, ikiwa ni pamoja na ubakaji, kudhuru mwili, biashara ya binadamu na utumwa wa kingono, imesema Ofisi ya Mashtaka ya Crown (S) siku ya Jumatano.
S imesema imeidhinisha mashtaka dhidi ya Andrew Tate, ambayo ni kutoka kwa walalamikaji watatu, kabla ya kibali cha kurejeshwa Uingereza kutoka Romania kutolewa mwaka 2024.
Kaka yake Tristan Tate anakabiliwa na mashtaka 11, ikiwa ni pamoja na ubakaji, kudhuru mwili na biashara ya binadamu, kutoka kwa mlalamikaji mmoja.
Ndugu hao daima wamekanusha makosa yoyote.
S ilisema katika taarifa yake kwamba mahakama nchini Romania, ambako wanachunguzwa kwa makosa ya jinai, iliamuru warejeshwe Uingereza mwaka jana.
"Hata hivyo, masuala ya uhalifu wa ndani nchini Romania lazima yatatuliwe kwanza," alisema msemaji wa S.
Ndugu hao walisafiri kwa ndege kwenda Marekani mwezi Februari baada ya waendesha mashtaka wa Romania kuondoa marufuku ya kusafiri, na kisha wakarudi Romania mwezi uliofuata ili kutimiza majukumu ya kisheria.
Kando na kesi hiyo, Andrew Tate pia anakabiliwa na kesi ya madai nchini Uingereza , ambayo imefunguliwa na wanawake wanne na anatazamiwa kufikishwa mahakamani mwaka 2027.
Daktari mstaafu jela kwa kubaka mamia ya wagonjwa wakiwemo watoto
Chanzo cha picha, CNN
Maelezo ya picha, Daktari wa zamani wa upasuaji amekiri kuwanyanyasa kingono mamia ya watoto nchini Ufaransa Daktari mstaafu wa upasuaji huko Ufaransa ambaye aliwanyanyasa kingono mamia ya wagonjwa vijana, wengi wao wakiwa watoto, kwa zaidi ya miongo miwili amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela siku ya Jumatano.
Joel Le Scouarnec alishitakiwa kwa ubakaji au unyanyasaji wa kingono kwa waathiriwa 299, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa baadhi ya watoto wakati wakiwa hawajifahamu. Aliiambia mahakama kuwa alifanya "vitendo vya kuchukiza" katika kipindi cha miaka 25 alipokuwa akifanya kazi kama daktari magharibi mwa Ufaransa.
Jaji Kiongozi Aude Buresi, alisema, "matendo yako yalikuwa doa katika ulimwengu wa matibabu.”
Le Scouarnec tayari anatumikia kifungo kwa makosa ya awali ya ubakaji. Mwaka 2020, alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia wa mtoto wa jirani, pamoja na wapwa zake wawili na mgonjwa wa miaka minne.
Jaji pia amempiga marufuku Le Scouarnec kufanya kazi ya udaktari au kuwasiliana na watoto. Mahakama pia imeamuru awekwe kwenye sajili ya wahalifu wa ngono.
Pia unaweza kusoma:
Klabu ya Man Utd yazomewa baada ya kushindwa huko Malaysia
Chanzo cha picha, REUTERS
Kocha mkuu wa klabu ya Manchester United, Reuben Amorim anaamini itawasaidia vyema wachezaji wake kuondoka Kuala Lumpur huku sauti za kuzomewa zikisikika masikioni mwao baada ya kufungwa 1-0 na timu ya ASEAN All-Stars.
Baada ya kukata tamaa katika kampeni kali ya Ligi Kuu ya Premier kwa ushindi dhidi ya Aston Villa siku ya Jumapili, Man United ilisafiri maili 6,600 hadi Malaysia na kukosa afueni ya matatizo yanayowakumba.
Chini ya saa 24 baaada ya mshambuliaji wa Klabu ya Wolves Matheus Cunha kuruhusiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kukamilisha uhamisho wa dau la £62.5m kujiunga na United, Mkosi wa mabao uliwakumba tena katika mechi ya kwanza ya ziara ya baada ya msimu uliopita barani Asia.
Wakiwa katika hali ya nyuzi joto 30 na unyevu wa juu, kikosi cha Amorim kilishindwa kutumia fursa au nafasi kadhaa walizopata licha ya mabadiliko ya wachezaji ya mara kwa mara hali iliyomaanisha kuwa waliishia kutumia wachezaji 25 wa ziada.
Bao la kipindi cha pili kutoka kwa winga wa Myanmar Maung Maung Lwin lilitosha kuipa ushindi timu hiyo ya kusini Mashariki mwa bara Asia mbele ya mashabiki 72,550 waliohudhuria katika Uwanja wa Bukit Jalil, na kuzua kuzomwa na baadhi ya mashabiki kutoka moja wakati wa filimbi ya mwisho ya mechi mbao walikuwa wamelipa hadi pauni 260 kutazama United kwenye ziara yao ya kwanza Malaysia tangu 2009.
"Siku zote ninahisi hatia kwa uchezaji wa timu yangu tangu mchezo wa kwanza nilipowasili hapa," alisema Amorim.
Wanafunzi 'wanajuta' kutuma maombi katika vyuo vikuu vya Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump ametekeleza sera kali dhidi ya baadhi ya vyuo vikuu nchini Marekani kikiwemo cha Harvard. Wanafunzi kote duniani wana wasiwasi na wako katika hali ya sintofahamu, baada ya utawala wa Trump kuweka mipango ya kusitisha kwa muda kutoa viza kwa wanafunzi kusoma Marekani.
Taarifa rasmi ya Trump, inaamuru kusitishwa kwa muda kutoa viza wakati serikali ikijiandaa kuongeza uhakiki wa maombaji kupitia mitandao ya kijamii kwa wanaotuma maombi ya viza za wanafunzi.
Baadhi ya wanafunzi wameambia BBC, mkanganyiko huo umewafanya watamani wangetuma maombi katika vyuo nje ya Marekani.
"Tayari najuta," anasema mwanafunzi wa uzamili mwenye umri wa miaka 22 kutoka Shanghai, China ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa hofu ya kuhatarisha viza ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania.
"Hata nikisoma Marekani, huenda nikafukuzwa kurudi China bila kupata shahada yangu," anasema.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa kusitisha viza za wanafunzi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tammy Bruce aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne: "Tunachukua kwa uzito mkubwa mchakato wa kuhakiki nani anayekuja nchini, na tutaendelea kufanya hivyo."
Oliver Cropley, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 27 kutoka Norwich, Uingereza, anasema anapaswa kusoma Kansas Marekani kwa mwaka mmoja, lakini mpango huo sasa uko hatarini.
Mwanafunzi mwingine kutoka Jiji la Guangzhou, ambaye hakutaka jina lake litajwe, anayendesha kikundi cha ushauri kwa wanafunzi wa China wanaotaka kusoma Marekani, anasema hawaelewi jinsi ya kuwashauri waombaji kwa sababu sheria zinaendelea kubadilika.
Zaidi ya wanafunzi milioni 1.1 wa kimataifa kutoka zaidi ya nchi 210 waliandikishwa katika vyuo vya Marekani katika mwaka wa shule wa 2023-24, kulingana na Open Doors, shirika linalokusanya data za wanafunzi wa kigeni.
Pia unaweza kusoma:
Elon Musk aondoka Ikulu ya White House, atangaza DOGE kuendelea
Chanzo cha picha, Getty Images
Elon Musk, bilionea na mmiliki wa X (zamani Twitter), amethibitisha kuondoka kwake kutoka serikali ya Rais Donald Trump. Musk alikuwa akiongoza juhudi kubwa za kupunguza ukubwa na matumizi ya serikali ya Marekani, zilizosababisha maelfu ya nafasi za kazi za serikali kufutwa. Katika chapisho lake kwenye X, Musk alimshukuru Trump kwa fursa ya kusaidia kuendesha Idara ya Ufanisi Serikalini, inayojulikana kama DOGE.
Ikulu ya White House ilianza "kumwondolea" Musk nafasi yake kama mfanyakazi maalum wa serikali Jumatano usiku.Jukumu lake lilikuwa la muda mfupi na kuondoka kwake hakukutarajiwa, lakini linakuja siku moja baada ya Musk kukosoa mswada mkuu wa bajeti ya Trump, ambao unapendekeza kusitishwa kwa kodi ya mamilioni ya dola na ongezeko la matumizi ya ulinzi.
Musk alieleza kuwa muda wake kama mfanyakazi maalum wa serikali umefikia kikomo, na akaeleza shukrani zake kwa Rais Trump kwa fursa ya kupunguza matumizi mabaya. Alisisitiza kuwa "DOGE itaendelea kuimarika kadiri inavyokuwa sehemu ya maisha katika serikali nzima," akionyesha imani yake katika kuendelea kwa mradi huo.
Mjasiriamali huyo wa teknolojia mwenye asili ya Afrika Kusini alikuwa ameteuliwa kama "mfanyakazi maalum wa serikali," akifanya kazi ya shirikisho kwa siku 130 kila mwaka. Licha ya kuondoka kwake kukaribiana na kikomo hicho cha muda, taarifa za kuondoka kwake zilikuja baada ya kueleza kukata tamaa na mswada wa bajeti wa Trump, ambao alihofia utaongeza nakisi ya shirikisho na kudhoofisha kazi ya DOGE.
Kulingana na makadirio, takriban wafanyakazi 260,000 kati ya milioni 2.3 wamepoteza kazi zao au kukubali mikataba ya kuacha kazi kwa hiari kutokana na mradi huo wa DOGE. Katika baadhi ya matukio, majaji wa shirikisho walisitisha kufukuzwa kazi kwa wingi na kuamuru wafanyakazi waliofukuzwa kurejeshwa kazini.
Mahakama ya Biashara Marekani yasema Trump alikiuka mamlaka yake kutoza ushuru karibu kila nchi
Chanzo cha picha, Reuters
Mahakama ya Manhattan ya Biashara ya Kimataifa ilitoa uamuzi kuhusu kesi dhidi ya Trump na kusema kuwa alikiuka mamlaka yake akitumia sheria ya dharura kutoza ushuru karibu kila nchi.
Uamuzi huo ni pigo kubwa kwa moja ya sera muhimu za kiuchumi za Trump.
Utawala wake tayari umekata rufaa.
Mahakama ilikubaliana na kikundi cha wafanyabiashara na muungano wa maofisa wa serikali ambao walikuwa wamewasilisha kesi mbili tofauti.
Mahakama hiyo iliamua kwamba sheria "haimruhusu" kutumia agizo la rais kutoza ushuru.
Kuna fursa ya kukata rifaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama ya Rufaa ya Marekani huko Washington, D.C., na hatimaye katika Mahakama Kuu ya Marekani. Mara moja, Ikulu ya White House ilitoa ombi la kukata rufaa.
Soma zaidi:
Ghala la chakula Gaza lavamiwa na 'makundi ya watu wenye njaa' - WFP
Chanzo cha picha, EYAD BABA/AFP
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linasema kuwa "makundi ya watu wenye njaa" wamevamia ghala la usambazaji wa chakula katikati mwa Gaza.
Watu wawili wanaripotiwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa, shirika hilo lilisema, na kuongeza kuwa bado linathibitisha maelezo zaidi.
Video kutoka kwa shirika la habari la AFP ilionyesha umati wa watu wakiingia kwenye ghala la al-Ghafari huko Deir al-Balah na kuchukua mifuko ya unga na katoni za chakula huku milio ya risasi ikisikika. Haikujulikana mara moja milio hiyo ya risasi ilikuwa ikitokea wapi.
Katika taarifa yake, WFP ilisema mahitaji ya kibinadamu huko Gaza yalikuwa yamefikia kiwango "wasichoweza kudhibiti" baada ya Israel kuzuia misaada kuingia eneo hilo kwa karibu miezi mitatu.
Soma zaidi:
Trump 'ampa wiki mbili' Putin kuhusu hatma ya mzozo wa Ukraine
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump ameonekana kumuwekea Vladimir Putin makataa ya wiki mbili, akitishia kuchukua mkondo tofauti ikiwa mwenzake wa Urusi bado ataendelea kumrejesha nyuma kwa vitendo vyake.
Wakati Urusi ikizidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine, Trump aliulizwa katika Ikulu siku ya Jumatano ikiwa alifikiri Putin anataka kumaliza vita.
"Siwezi kukuambia hilo, lakini nitawajulisha baada ya wiki mbili," Trump aliwaambia waandishi wa habari huku kukiwa na msururu wa matamshi yaliyotolewa hadharani na Trump akimkosoa Putin.
Tangu Jumapili, Trump amekuwa akiandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema kwamba Putin amekuwa "mwendawazimu" na "anacheza na moto" baada ya Urusi kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 29/05/2025.